Matumizi ya dawa kuandikwa kwa Kiswahili

0
210

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ameagiza majina ya barabara, mitaa, mabango, fomu za usaili na maelekezo ya matumizi ya dawa pamoja na bidhaa na huduma viandikwe kwa lugha ya Kiswahili.

Dkt. Mpango ametoa agizo hilo mkoani Dar es Salaam katika maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani.

Pia amezitaka wizara na taasisi za serikali kuendelea kutekeleza maagizo ya serikali ya nyaraka za mawasiliano za wizara na idara ziwe kwa lugha ya Kiswahili na mikutano warsha, semina, mijadala ya umma na dhifa ziendeshwe kwa lugha ya Kiswahili

Aidha Dkt. Mpango amesema taarifa za miradi na mikataba inayohusu wananchi ni lazima ziandikwe kwa lugha ya Kiswahili na zisiwe kwa lugha za kigeni pekee.

“Sheria na kanuni ambazo bado hazijatafsriwa zitafsiriwe na wizara na taasisi zinazosimamia sheria na kanuni hizo kwa kushirikiana na mabaraza ya kiswahili, wataalam wengine wa kiswahili na ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali” ameagiza Dkt. Mpango

Hata hivyo Dkt. Mpango ameagiza vyombo vya habari nchini vinavyotumia lugha ya Kiswahili vihakikishe vinatumia kiswahili fasaha.

Dkt. Mpango amesisitiza Balozi zote zianzishe vituo vya kujifunzia lugha ya Kiswahili na ziwatumie wataalam wa lugha ya Kiswahili waliosajiliwa na kanzi data ya Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA).

Katika maadhimisho hayo ya Siku ya Kiswahili Duniani, Dkt. Mpango ameshuhudia Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda na Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini, Angelina Motshekga wakisaini hati za makubaliano ya Kiswahili kufundishwa katika shule za msingi za nchini Afrika Kusini.