Wizara ya Ardhi yazuia upangaji ardhi Monduli

0
125

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula amezuia mkataba wa upangishaji ardhi wa mashamba matatu maarufu kama mashamba ya Steyn yaliyopo wilayani Monduli mkoani Arusha ulioingiwa kati ya halmashauri ya wilaya ya Monduli na kampuni ya EBN Hunting Safaris.
 
Uamuzi huo unafuatia halmashauri ya wilaya ya Monduli kuingia mkataba wa kufanya uwekezaji kwenye mashamba hayo ulioibua mkanganyiko baina ya ofisi ya Msajili wa Hazina na halmashauri ya wilaya ya Monduli kutokana na ofisi ya Msajili kutokamilisha wala kutoa shamba hilo  kwa mtu ama mamlaka yoyote.
 
Hatua ya halmashauri kutafuta mwekezaji kwenye mashamba hayo ilitokana na ufutwaji mashamba uliofanywa na Rais wa serikali ya awamu ya tatu Hayati Benjamin Mkapa kupitia tangazo la serikali la mwaka 2005 kwa lengo la upanuzi wa mji wa Makuyuni.
 
Mashamba ya Steyn ni muunganiko wa mashamba matatu ya Lente estate, Amani na Loldebes yenye ukubwa wa ekari 15,163, ambapo miaka ya 70 raia waliomiliki mashamba hayo waliondoka nchini na kuyaacha kumilikiwa na Hermanus Steyn kupitia kampuni ya Rift Valley Seed Company Ltd.
 
Akitoa uamuzi huo baada ya kukagua mashamba hayo wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani Arusha, Dkt Mabula amesema mashamba hayo kwa mujibu wa sheria ya utwaaji yako chini ya umiliki wa Msajili wa Hazina, hivyo uongozi wa wilaya ya Monduli ulitakiwa kuomba kibali cha matumizi ya eneo baada ya kutwaliwa.