Morrison arejea Yanga

0
186

Mchezaji wa Kimataifa wa Ghana, Bernard Morrison rasmi amerejea kwenye Klabu yake ya zamani, Yanga SC akitokea Simba SC baada ya kumaliza mkataba wake na Wekundu hao wa Msimbazi alipoanza kucheza tangu mwaka 2020.

Morrison aliondoka Yanga SC kwa sekeseke la utata wa mkataba baina yake na Wananchi, ambapo Simba SC walimsajili wakidai alikuwa hana mkataba na timu hiyo yenye maskani yake mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, baada ya kucheza Soka ndani ya Simba SC katika mkataba wake wa miaka miwili baadae, Morrison aliondoka klabuni hapo ikidaiwa anaenda kumaliza masuala yake ya kifamilia nyumbani kwao, nchini Ghana.

Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Barbara Gonzalez hivi karibuni alinukuliwa kwenye baadhi ya Vyombo vya Habari akisema kuwa hatotoa barua (Release Letter) ya kuachana na Mchezaji huyo hadi atakapomaliza mkataba rasmi na Klabu hiyo ya Simba SC au timu inayomhitaji kwenye kipindi hicho cha kumalizia mkataba wake, iiandikie barua Simba SC kuhitaji huduma yake.

Julai 4, 2022, siku ya Jumatatu Usiku wa Saa 6:01, Yanga SC wametangaza kumrejesha Mchezaji huyo Jangwani licha ya awali kuzua sekeseke kubwa la mkataba wake na kupelekea kusajiliwa na Simba SC.