Askari Uhifadhi watakiwa kujenga uhusiano mzuri na wananchi

0
178

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja (Mb) amewataka askari wa uhifadhi nchini kujenga mahusiano mazuri na jamii inayozunguka maeneo ya hifadhi wanazozisimamia kwa kufanya kazi kwa kushirikiana nao katika masuala mbalimbali.

Ameyasema hayo leo mkoani Kilimanjaro katika ziara ya kikazi alipotembelea Shamba la Miti la West Kilimanjaro na kusema jamii inapokuwa hairidhishwi na utendaji kazi wa wahifadhi kunakuwa na migongano inayoipelekea wahifadhi kuchukiwa na wananchi.

“Jamii ikiwa haina mahusiano mazuri hata ninyi haya mashamba hamuwezi kuyaendeleza vizuri, kwa hiyo lazima muhakikishe mnajenga mahusiano mazuri,” Masanja amesisitiza.

Aidha, amewataka wahifadhi wanaozunguka mlima Kilimanjaro kupanda miti kuzunguka mlima huo na kuhakikisha wanagawa miche ya miti kwa wananchi ili kuuzuia mlima usiendelee kuyeyuka.