Wanahabari wafundwa kuhusu gesi asilia

0
157

Wahariri pamoja na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari kutoka mkoani Dar es Salaam wamefanya ziara ya kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu masuala ya uchakataji wa gesi asilia.

Waandishi hao wametembelea eneo la Msimbati mkoani Mtwara ambako kunapatikana visima vya uchimbaji wa gesi asilia pamoja na Madimba ambako kuna kiwanda cha kuchakata gesi asilia.

Wanahabari hao wamesema ziara hiyo ni imewasaidia kufahamu kwa kina rasilimali muhimu ya nchi ambayo inaongeza tija na uchumi kwa taifa na namna gani kazi zinavyofanyika.

Aidha, wamesema gesi asilia ni rasilimali muhimu kwa Watanzania ambayo imekuwa ikitumika katika matumizi mbalimbali kama vile uzalishaji wa umeme pamoja na kuendeshea magari.

Kaimu Mhariri Mkuu wa TBC, Anna Mwasyoke amesema “Waandishi wa habari na wahariri ni daraja kati ya wananchi na wale wenye mamlaka kwa hiyo wakifahamu vizuri kuhusu rasilimali za taifa wataweza kuandika taarifa kwa usahihi zaidi kwa maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.”

Ziara hiyo imeandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) ambapo Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Wadau, Charles Change amesema waandishi wa habari ni wadau wakubwa na wanategemewa katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa sahihi za gesi asilia kwa wananchi.