Viongozi wa mitaa wanolewa kuhusu elimu ya uhifadhi wa mikoko

Semina

0
167

Mabalozi, wenyeviti wa serikali za mitaa na maafisa mifugo na maliasili kutoka wilaya ya Kinondoni wametakiwa kusimamia rasilimali za mikoko na kutumia sheria ndogo ndogo na makatazo ili kulinda mikoko na kutumia rasilimali hiyo katika kutengeneza miundombinu ya kuvutia utalii na watalii nchini

Wakala wa huduma za misitu (TFS) wametoa mafunzo kuhusu elimu ya misitu na mikoko kwa watendaji na viongozi wa mitaa waliokaribu na maeneo ya misitu ili kuendelea kulinda rasilimali za misitu na matumizi ya sheria ndogo katika kutoa adhabu kuhusiana na rasilimali za misitu ikiwa ni pamoja na kutumia fursa hiyo katika kutengeneza miundombinu ya kutangaza utalii wa mikoko nchini Tanzania

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika Kunduchi Mkoani Dar es salaam Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni Stella Msofe, akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya Hiyo Godwin Gondwe amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa viongozi hao na kuwataka kwenda kuwa mabalozi kwa jamii na viongozi wengine pamoja na wawekezaji ili kuipa hadhi misitu na rasilimali ya mikoko katika kuchangia kwenye pato la taifa kupitia utalii

‘’Kwa sasa tunaweza kutumia mafunzo haya kujiongezea fursa katika kuifanya rasilimali hii ya mikoko kuwa kivutio kikubwa cha utalii katika wilaya yetu ya Kinondoni” amesema Msofe

Akizungumza baada ya mfunzo hayo Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbweni Hasna Hussein Amesema mafunzo hayo yatawasaidia katika kukabiliana na kusaidia kutatua changamoto za mikoko ikiwemo mipaka ya mikoko na usimamizi wa rasilimali za misitu iliyopo katika wilaya ya kinondoni