Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Juni 23, 2022 ameshiriki zoezi la awamu ya pili ya wananchi takribani 117 kutoka kaya 27 wanaohama kwa hiari kutoka katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro kuelekea kijiji cha Msomera, Handeni mkoani Tanga.
Waziri Mkuu Majaliwa amewapongeza wakazi hao kwa maamuzi yao ya kuhamia katika kijiji cha Msomera ambapo amewahakikishia kwamba Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ipo pamoja nao.
“Nataka niwaambie nyie mna bahati sana kwa maana kule mnapohamia kuna kila kitu hivyo mnakwenda kuanza maisha mapya kwenye eneo ambalo limeandaliwa vizuri.” amesema Waziri Mkuu
Pia ametoa salamu za Rais kwa wananchi hao ambapo amewatakia heri katika maisha mapya na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kuwa pamoja nao.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Majaliwa atakagua alama zilizowekwa kubainisha eneo la hifadhi ya pori tengefu la Loliondo la kilomita za mraba 1,500 na eneo la wananchi kilomita za mraba 2,500.