Baa ya vioo inayoning’inia kwenye korongo

0
4211

Huenda ukahitaji kinywaji kabla hata ya kufika kwenye baa ama kusimuliwa kuhusu baa ya maajabu iliyopo huko nchini Georgia.

Ni kwamba baa hiyo yenye umbo la almasi imejengwa katikati ya daraja la vioo lenye urefu wa mita 240 (futi 787) katika eneo la Dashbashi Canyon.

Kama unatoka mji mkuu wa Georgia, Tbilisi na unataka kufika katika eneo ilipo baa hiyo ya maajabu unalazika kutumia muda wa saa mbili kwa mwendo wa gari.

Daraja hilo la vioo limebuniwa na kujengwa na wawekezaji kutoka kampuni ya Kass inayofanya shughuli zake katika nchi ya Georgia pamoja na Israel kwa dola milioni 40 za Kimarekani.

Baa yenyewe iliyopo kwenye daraja hilo imejengwa kwa kutumia chuma na glasi na imechukukua muda wa takribani miaka mitatu ili kukamilisha ujenzi huo.

Kitu kinachoelezwa kuwa ni cha kipekee katika baa hiyo ni uwepo wa ngazi katika eneo lake la juu kabisa, na kulifanya jengo la baa hiyo kuwa kubwa na refu zaidi la kuning’inia kuliko yote duniani.

Ukumbi wa baa hiyo umeripotiwa kuingizwa katika rekodi za dunia za Guinness.

Ukiwa katika daraja hilo la vioo hasa ndani ya baa hiyo ya maajabu unaweza kushuhudia mandhari nzuri, kuvuka korongo pamoja na mwamba na pia kubembea.