Bilioni 195 kupeleka maji Shinyanga

0
130

Serikali ya Ufaransa kupitia shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), imetia saini mkataba wa kuipatia Tanzania mkopo wa Euro milioni 75 sawa na takribani shilingi bilioni 195 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa usambazaji majisafi na usafi wa mazingira katika mkoa wa Shinyanga. 

Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo mkoani Dar es Salaam Katibu Mkuu wizara ya Fedha na Mipango Emmanuel Tutuba amesema, lengo la mradi huo ni kutoa huduma za uhakika na endelevu za upatikanaji wa majisafi na usafi wa mazingira katika manispaa ya Shinyanga.

Amesema mradi huo utaboresha afya, ustawi wa jamii na hali za maisha ya wanufaika wa mradi huo kwa kuboresha na kuimarisha miundombinu iliyopo na kuongeza ufanisi wa uendeshaji na utoaji wa huduma bora kupitia Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA). 

Mradi huo ukikamilika utaongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa asilimia 95 katika manispaa ya Shinyanga na baadhi ya miji midogo katika wilaya ya Shinyanga na utawanufaisha wananchi zaidi ya laki tatu.