Aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake wanne wamefikishwa tena katika mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi hii leo, kujibu tuhuma mbalimbali zinazowakabili ikiwemo uhujumu uchumi.
Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo Salome Mshasha, ambaye tarehe 7 mwezi huu aliiahirisha baada ya upande wa mashtaka kueleza kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Sylvester Nyegu, John Aweyo, Nathan Msuya na Antero Assey.
Kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa tarehe 7 mwezi huu, wakili wa upande wa utetezi Hellen Mahuna aliiomba mahakama hiyo ya Hakimu Mkazi Moshi kuharakisha upelelezi kwa kuwa mteja wake ambaye ni Sabaya ni mgonjwa, kutokana na uvimbe alionao kichwani ambao anatakiwa kufanyiwa upasuaji.