Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi amewataka Maafisa Waandamizi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kufanya jitihada kubwa za kuzuia mianya ya rushwa kabla haijatokea.
Ndejembi ametoa kauli hiyo wilayani Kibaha mkoani Pwani wakati akifunga mafunzo ya maafisa hao kwa ajili ya kuwajengea uelewa na utimamu kazini ambapo amewataka kuwa waadilifu na wazalendo kwa Nchi yao.
“TAKUKURU mnafanya kazi nzuri lakini niwatake kutumia mafunzo haya ya uongozi mliyoyapata kwenda kuhakikisha mnatekeleza maelekezo ya Rais Samia lakini vilevile mnafuata Sheria, Taratibu na Kanuni katika kufanya majukumu yenu. Na zaidi endeleeni kutoa elimu kwa wananchi ili tuwajengee watu wetu uelewa mpana wa kuona rushwa ni kitendo kisicho cha kizalendo na waichukie,” amesema.
Amesema TAKUKURU haipaswi kusubiri mpaka viongozi wakuu watembelee miradi ndio waone kuna ubadhirifu watoe maelekezo kwao.
“Rais Samia anatekeleza miradi mikubwa kila kona ya Nchi yetu ni jukumu lenu kumuunga mkono kwa kuisimamia ili asiwepo mtu ambaye atajinufaisha tumbo lake,” amesisitiza Ndejembi.