Vigezo vya uanzishaji vituo vya polisi vyatajwa

0
188

Serikali imesema vigezo vinavyotumika kuanzisha vituo vya polisi ni pamoja na ongezeko la watu, matukio ya uhalifu na umbali kati ya kituo kimoja cha polisi na kingine.

Vigezo vingine ni uwepo wa miundombinu ya serikali, shughuli za kibiashara pamoja na maeneo ya kimkakati kwa ajili ya ulinzi na usalama wa nchi.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Jumanne Sagini wakati akijibu swali la Mohamed Jumah Soud mbunge wa jimbo la Donge lililopo Zanzibar aliyetaka kufahamu ni vigezo gani hutumika kusnzisha vituo vya polisi kwenye maeneo yenye idadi kubwa ya watu.

“Uwezo wa Kibajeti na utayari wa wananchi na mamlaka zao za serikali za mitaa ni vigezo vingine tunavyovitumia.” ameongeza Naibu Waziri Sagini

Amesema hatua inayofuata ni mapendekezo ya uanzishwaji wa kituo husika kuwasilishwa kwa kamati ya usalama ya wilaya na ya mkoa na kisha ushauri wao huwasilishwa kwa mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kwa ajili ya utekelezaji.

Naibu Waziri Sagini amesema kama jimbo la Donge linakidhi vigezo hivyo, anamuelekeza Kamishna wa Polisi Zanzibar kufanya tathmini ya eneo hilo na akibaini linakidhi vigezo ujenzi wa kituo cha polisi ufanyike.