Bilioni 66 zakusanywa daraja la Nyerere

0
199

Hadi kufikia mwishoni.mwa mwezi Mei mwaka huu, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ulikuwa unekusanya shilingi bilioni 66.86 zikiwa ni fedha zitokanazo na tozo kwa watumiaji wa daraja la Nyerere mkoani Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Godfrey Kasekenya amesema
NSSF ilianza kupokea fedha Mei 14 mwaka 2016 baada daraja hilo kuzinduliwa.

Amesema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa jimbo la Kigamboni mkoani Dar es Salaam, Dkt. Faustine Ndugulile alilyetaka kufahamu ni kiasi gani cha fedha kimekusanywa tangu daraja hilo la Nyerere lianze kutumika.

Naibu Waziri Kasekenya amesema serikali imeendelea kupunguza tozo kwa watumiaji wa daraja hilo tangu kuzinduliwa kwake kwa kuzingatia tathmini ya uwezo wa wananchi kumudu tozo hizo, na kwamba kwa mara ya mwisho serikali imepunguza tozo husika Mei 21 mwaka huu.

Akijibu swali la nyongeza la Dkt. Ndugulile, Naibu Waziri Kasekenya amesema, serikali inakamilisha mfumo wa kuanza tozo kwa siku, kwa wiki na kwa mwezi na inategemea kuanzia Julai Mosi mfumo huo uanze kutumika.