Nape aagiza waliozusha kupande bei ya umeme wawajibishwe

0
151

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameagiza hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wale wote waliohusika kusambaza taarifa za uongo kuwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limepandisha bei za umeme.

Nape ametoa maelekezo hayo kupitia ukurasa wake wa Twitter akisema kuwa “utungaji na uenezaji wa taarifa za uongo kiasi hiki ni uchochezi wenye lengo la kujenga chuki dhidi ya TANESCO na Serikali.”

Agizo lake limekuja saa chache baada ya Waziri wa Nishati, January Makamba kuziomba mamlaka husika kuchukua hatua stahiki kwa wale wote wanaovumisha taarifa hiyo ya uzushi kuhusu kupanda kwa bei ya umeme nchini.

Makamba amesema mchakato wa kupanda au kushuka kwa bei ya umeme si mchakato wa siku moja na wala haufanywi kwa siri, bali mchakato huu huusisha maombi ya TANESCO kwa EWURA na pia ni lazima Wananchi wahusishwe ili kutoa maoni yao ndipo mchakato ukamilike.