Byabato: Mafuta hayajashuka, yameshushwa

0
252

Naibu Waziri wa Nishati Steven Byabato amesema duniani bei ya mafuta haijashuka isipokuwa hapa nchini bei hizo zimeshushwa na Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na ruzuku aliyoitoa kupunguza makali ya bei hizo.

Akizungumza na wananchi wa mkoa wa Kagera waliojitokeza katika uwanja wa Kaitaba kumlaki Rais Samia Suluhu Hassan, Naibu Waziri Byabato amesema kwa sasa kuna unafuu mkubwa wa bei za mafuta hapa nchini kutokana na ruzuku ya shilingi bilioni 100 aliyotoa Rais.

“Napenda kuwaambia wananchi wa mkoa wa kagera kuwa bei za mafuta kwa hapa kwetu ingekuwa imefika 3,600 lakini kutokana na ruzuku aliyotoa Rais wetu bei hizo zimebakia 3,300 ama 3,200 na imekuwa ni nafuu sana kwetu” amesema Naibu Waziri Byabato

Aidha amemshukuru Rais Samia kwa namna ambavyo amekuwa mstari wa mbele katika kupeleka fedha za maendeleo kwenye jimbo lake ikiwa ni pamoja na kupeleka fedha katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Kagera na miradi mingine ya barabara, maji, elimu na miundombinu.