Serikali imefuta kodi ya pango ya
ardhi kwa taasisi na madhehebu ya dini nchini kuanzia mwaka wa fedha wa
2018/2019.
Hatua hiyo imetangazwa jijini Mbeya na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, – William Lukuvi wakati wa ibada ya kuwaweka Wakfu viongozi wa Jumuiya
Kuu ya Kanisa la Kibaptisti Tanzania (BCT).
Akitangaza hatua hiyo, Waziri Lukuvi
amesema kuwa Rais John Magufuli ameiagiza wizara hiyo kutoyatoza
kodi madhehebu ya dini kwa sehemu ambazo zimeandaliwa kwa ajili ya kufanyia
ibada.
“Rais ameagiza kuanzia Julai mosi mwaka huu wa fedha, madhehebu ya dini yasilipe kodi ya ardhi kwa
maeneo ambayo huduma za maombi na ibada zinatolewa, hata hivyo msamaha huu
hauhusu maeneo ambayo kuna miradi ya kuingiza fedha ambayo tunajua madhehebu
mengi yameanzisha,” amesema Waziri Lukuvi.
Amefafanua kuwa tayari agizo hilo limetolewa kwa Makamishna wa ardhi wa kanda
na mikoa pamoja na maofisa ardhi wa majiji, manispaa na halmashauri zote nchini.
Hata hivyo, Waziri Lukuvi ametoa nafasi
ya kukutana na viongozi wa dini ambao wana migogoro ya ardhi kwenye maeneo
ambayo wanatoa huduma.
“Najua kuna migogoro mingi kwenye maeneo ambayo mnatoa huduma, hivyo nawakaribisha ofisini kwangu Dodoma na
kama migogoro itakuwa mikubwa nitafika mpaka eneo la mgogoro,” amesema Waziri
Lukuvi.
Awali, Askofu wa kanisa la Baptisti nchini, Arnold Manase alimweleza Waziri
Lukuvi kuwa kanisa hilo ni moja ya
madhehebu yanayoongoza kwa kuwa na migogoro ya ardhi.
“Kwa kuwa Waziri mwenye dhamana upo, naomba nafasi nije ofisini kwako
nikueleze migogoro iliyopo ndani ya kanisa langu ili uangalie namna ya kuitatua
maana migogoro imekithiri mpaka kufikia hatua ya kujenga makundi miongoni mwa
waumini,” amesema Askofu Manase.