Bunge laidhinisha bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii

0
145

Bunge la Bajeti likiendelea jijini Dodoma, leo Juni 03, 2022 limeidhinisha shilingi bilioni 620 ya matumizi ya Fungu 69 la Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Akitoa hotuba Waziri, Balozi Dkt. Pindi Chana amesema kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 443 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 180 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Aidha, hotuba hiyo imeeleza kuwa Tanzania imeendelea kutambulika kimataifa na kupata tuzo mbalimbali zikiwemo Hifadhi ya Taifa Serengeti kuwa hifadhi inayoongoza kwa ubora Barani Afrika kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2019 hadi 2021

Wizara imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake kubwa za kuitangaza nchi kimataifa kupitia programu ya Tanzania: The Royal Tour.

“Programu hiyo imewezesha kuitambulisha Tanzania kimataifa kwa kutangaza vivutio vya utalii vya kipekee vya nchi yetu; kuonesha fursa mbalimbali za uwekezaji kwenye sekta ya maliasili na utalii pamoja na kuimarisha nafasi ya nchi katika jumuiya za kimataifa,” amesema Balozi Chana.

Wizara imesema itaendelea kuongeza jitihada za kuimairisha ulinzi na uhifadhi wa rasilimali za maliasili kwa kudhibiti ujangili, biashara haramu ya nyara, uvunaji haramu wa mazao ya misitu na uvamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa, jitihada hizo zinadhihirishwa na matokeo ya sensa ya wanyamapori iliyofanyika mwaka 2021 ambapo idadi ya tembo imeongezeka kwa asilimia 30 katika Mfumo Ikolojia Ziwa Natron – West Kilimanjaro.