Tanzania na Ireland zimeahidi kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano ambayo ni biashara na uwekezaji, kilimo, viwanda vya nguo pamoja na ujenzi.
Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula alipokutana kwa mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Ireland, Joe Hackett katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Balozi Mulamula ameongeza kuwa kupitia biashara na uwekezaji wafanyabiashara wa Kitanzania watapata fursa ya kuchangamkia biashara zinazopatikana nchini Ireland lakini pia wafanyabiashara wa Ireland watapata fursa ya kuwekeza nchini Tanzania.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje wa Ireland, Joe Hackett amesema Ireland wamefurahishwa na hatua ambazo Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikizichukua katika kuimarisha na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji pamoja na kuinganisha Tanzania na mataifa mengine ulimwenguni.
Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ya uhusiano baina ya Tanzania na Ireland katika maeneo yenye maslahi kwa pande zote mbili.
Katika tukio lingine, Balozi Mulamula ameongoza kikao cha majadiliano ya mpango wa kuimarisha diplomasia ya uchumi ya Tanzania.