Kampuni ya Scania yaonesha nia kuwekeza sekta ya usafirishaji nchini

0
133

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango ametembelea makao makuu ya kampuni ya utengenezaji wa magari ya Scania iliyopo Stockholm nchini Sweden na kujionea teknolojia ya utengenezaji wa magari yanayotumia nishati ya gesi ikiwemo gesi inayotokana na taka ngumu, lengo likiwa ni kupunguza ongezeko la gesi joto duniani.

Dkt. Mpango amefanya mazungumzo na mkurugenzi wa teknolojia endelevu ya utengenezaji magari wa Kampuni ya Scania, Jonas Strömberg pamoja na mkuu wa teknolojia endelevu ya usafirishaji wa kampuni ya Scania Fredrik Wijkander, mazungumzo yaliolenga kuongeza ushirikiano baina ya Tanzania na Kampuni hiyo.

Amesema Tanzania ipo tayari kwa ajili ya ushirikiano na kampuni hiyo hasa katika vyuo vya ufundi vitakavyowezesha uhamilishaji wa teknolojia, na ameikaribisha kampuni hiyo kushirikiana na wafanyabiashara wa sekta ya usafiri ili kueneza teknolojia ya matumizi ya nishati mbadala katika usafirishaji na kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira.

Kwa upande wake Wijkander amesema Scania inavutiwa na mabadiliko mbalimbali yanayofanyika nchini Tanzania ikiwemo uboreshaji wa sekta ya uwekezaji ambayo inawapa hamasa ya kushirikiana na Tanzania katika sekta ya usafirishaji hususani usafiri wa mizigo na abiria.

Makamu wa Rais yupo nchini Sweden kuhudhuria Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Stockholm +50 wenye dhumuni la kuchochea utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (Ajenda 2030) hususani katika upande wa mazingira na kujadili namna ya kurejesha uchumi endelevu katika kukabiliana na janga la Uviko 19.