Mawakili wapewa siku 30 kuwa nia mihuri ya kielektroniki

0
749

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro ametoa siku 30 kwa mawakili wote kuhakikisha wanakuwa na mihuri mipya ya kielektoniki ili kuondoa malalamiko ya watu wanaojifanya mawakili (vishoka ) kwa kutumia mihuri ya mawakili hao.

Dkt. Ndumbaro ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Mawakili Tanzania (TLS) unaofanyika jijini Arusha na kuongeza kuwa baada ya hapo hawatatambua mihuri mingine yoyote ambayo sio wa kielektoniki.

“Tutaandikia mamlaka zote zinazotambua mihuri ya mawakili maelekezo ikiwemo TRA juu ya kuhakikisha mawakili wote wanakuwa na mihuri hiyo lengo likiwa ni kuondoa malalamiko ya watu wanaotumia mihuri ya mawakili,”ameongeza Ndumbaro.

Katika mkutano huo waziri Ndumbaro amezindua mihuri ya kielektoniki, na kizindua SACCOS ya mawakili.

Kwa upande wake Rais wa TLS, Dkt. Edward Hosea amesema mkutano huo umewakutanisha mawakili wote kutoka Tanzania ambao ni wanachama na wanatarajia kujadili mada ambazo zitaleta tija na ufanisi katika chama hicho.