Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amepiga marufuku uchinjaji wa punda Tanzania kutokana na hatari ya kutoweka kwa kizazi cha punda na idadi ya punda nchini kuendelea kupungua kama hatua za haraka hazitochukuliwa.
Waziri Ndaki amewataka Watanzania kuwatumia Punda kwenye matumizi ya kiuchumi lakini sio kitoweo.
Waziri Ndaki amesema nchi nyingi Duniani zimepinga marufuku biashara ya nyama ya punda kwa sababu wanapungua na punda wanazaliana kwa nadra sana ambapo wanawezachukuwa miaka mitatu au sita kuzaa.
Amesema “kwa sasa idadi ya punda ni takriban 650,000, katika mwaka 2021/2022 hivyo wizara imesitisha shughuli zote za biashara ya uchinjaji wa punda nchini”
“Napenda, kutumia fursa hii kuwataarifu wawekezaji waliowekeza katika machinjio ya punda nchini watumie miundombinu ya machinjio hizo kwa ajili ya kuchinja na kuchakata aina nyingine za mifugo hususan ng’ombe, mbuzi na kondoo.”Amesema Waziri Ndaki
Aidha Waziri Ndaki amesema wizara itaendelea kutambua na kusajili mifugo kwenye mfumo wa kielektroniki ili kufikia lengo la kusajili takriban mifugo 45,000,000 (ng’ombe, mbuzi, kondoo na punda) iliyopo nchini ifikapo Juni, 2023.
Waziri Ndaki ameyasema hayo wakati Bunge linapitisha bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka 2022/2023.