Prof. Shemdoe azinyooshea kidole Halmashauri 8

0
106

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe amezinyooshe kidole halmashauri 8 ambazo hazijatenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa afua za Lishe kwa mwaka wa fedha 2020/21.

Amezitaja Halmashauri hizo kuwa ni Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Halmashauri ya Mji Musoma, Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Halmashauri ya Momba na Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga.

“Naagiza Wakurugenzi wa Halmashauri hizo kuhakikisha wanatenga fedha hizo kabla ya kufunga mwaka wa fedha 2021/22 kwa kuwa wamekiuka mkataba uliwekwa na Serikali wa Kuhakikisha fedha hizo zinatengwa kwa wakati ili kupunguza utapia mlo nchini” amesema Prof.Shemdoe

Akifungua kikao cha kujadili utekelezaji wa Mkataba wa afua za lishe nchini kilichowashirikisha Waganga wakuu wa Mikoa, Maafisa lishe wa Mkoa na wadau wa lishe leo tarehe Mei 25, 2022 Prof. Shemdoe amesema kila Halmashauri inawajibu wa kutenga kiasi cha shilingi 1000 kwa kila mtoto aliye chini ya umri wa miaka mitano kwa ajili ya afua za lishe kama mkataba ulivyoelekeza.

Shemdoe amesema utengaji na upelekaji wa fedha za afua za lishe ni moja ya kigezo kitakachotumika kuwapima Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini lengo likiwa ni kuhakikisha tatizo la utapia mlo nchini linamalizika.

Akielezea kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali kuhusu utekelezaji wa afua za lishe nchini Shemdoe amesema Serikali inaendelea kusimamia uandaaji wa mpango wa bajeti za Halmashauri ili zitenge na kutumia shilingi 1000 kwa kila mtoto kwa kuwa ni moja ya kiashiria kilichoonyeshwa kwenye mkataba wa afua za lishe nchini.