Tume ya utumishi wa umma yatakiwa kutenda haki

0
140

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Deo Ndejembi ameielekeza Tume ya Utumishi wa Umma kushughulikia kwa wakati rufaa zilizowasilishwa, ili kuwawezesha warufani kupata haki zao kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma.

Naibu Waziri Ndejembi ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma wakati akizindua rasmi Tume ya Utumishi wa Umma, ambayo makamishna wake wameteuliwa na kuapishwa hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema tume hiyo ina rufaa na malalamiko mengi ambayo yanatakiwa kutolewa maamuzi, hivyo haina budi kuyashughulikia ili kutenda haki na kuondoa sintofahamu kwa warufani wanaosubiri hatma ya rufaa zao.

“Wengi wenu hapa makamishna ni wanasheria na katika sheria mnasema justice delayed is justice denied, hivyo mkayashughulikie hayo mashauri kwa wakati.” amesisitiza Naibu Waziri Ndejembi

Ameongeza kuwa, Tume ya Utumishi wa Umma isipofanya uamuzi sahihi na kwa wakati itaongeza malalamiko katika utumishi wa umma na kukwamisha shughuli za maendeleo na huduma muhimu ambazo zinazotolewa na waliowasilisha mashauri na rufaa zao.

Kuhusu utatuzi wa changamoto ya baadhi ya waajiri na warufani kutowasilisha vielelezo vya rufaa kwa wakati, Ndejembi amesema kuwa ofisi yake inafanya marekebisho ya kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2003 ambayo yataipa tume mamlaka ya kusikiliza na kutoa maamuzi ya rufaa kwa kutumia vielelezo vya upande mmoja vilivyopo.

“Kuna mashauri mengi Tume ya Utumishi wa Umma ambayo yanasababisha tume kulalamikiwa kwa kutotolea maamuzi wakati vielelezo vya mashauri hayo havijawasilishwa, hivyo tumeamua kurekebisha kanuni ili kuipa tume mamlaka ya kufanya maamuzi ya rufaa kwa kutumia vielelezo vilivyopo.” amefafanua Naibu Waziri Ndejembi