Wadau watoa ushauri kwenye sekta madini

0
1016

Wadau wa sekta ya madini nchini wameishauri serikali  kuwawezesha wachimbaji wadogo wa madini kwa kuondoa kodi mbalimbali ambazo zimekua zikiwaumiza ikiwa ni pamoja na Kodi ya Ongezeko la thamani (VAT).

Wadau  hao wametoa  ushauri huo jijini Dar es salaam wakati wa mkutano wa wachimbaji wadogo wa madini, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini, mkutano uliokuwa na lengo ya kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji wadogo wa madini na namna ya kuzitatua.

Wamesema kuwa kuwepo kwa kodi na tozo nyingi zinazotozwa na taasisi mbalimbali kunasababisha vitendo vya utoroshwaji wa madini.

Naye mmoja wa wadau hao Mutalemwa Titus amesema kuwa kwa  kipindi cha miaka mitatu wameshindwa kuuza madini yao kutokana na wizara ya Madini kuwakatalia kuyeyusha madini hayo aina ya Tin, hivyo kumuomba Rais Magufuli kuingilia kati suala hilo.

Muinjilisti Solomoni Mihayo ni Mdau wa madini kutoka mkoani Geita, yeye ametaja njia mbalimbali zinazoweza kutumiwa na watu wasio waaminifu kusafirisha madini nje ya nchi ikiwa ni pamoja na  madini yenye thamani kubwa kufungwa kwenye matairi ya akiba ya magari na  kuwekwa kwenye vioo vya kuongozea  magari.