Wizara ya ujenzi na uchukuzi yaomba trilioni 3.8

0
255

Serikalli imepanga kutumia shilingi bilioni 468 kutoka mfuko mkuu kwa ajili ya kutekeleza shughuli za kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) katika mwaka wa fedha wa 2022/2023.

Miongoni mwa shughuli zitakazotekelezwa ni kukamilisha malipo ya ununuzi wa ndege tano mpya ambapo ndege moja ni aina ya Boeing 787-8 Dreamliner, ndege mbili aina ya Boeing 737-9, ndege moja ya mizigo aina ya Boeing 767-300F na ndege moja aina ya Dash 8 Q400.

Hayo yamesemwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023.

Pia amegusia mikakati ya serikali kwa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) katika mwaka wa fedha wa 2022/2023.

“Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 1.77 kutoka mfuko mkuu wa serikali kwa ajili ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kutekeleza ununuzi wa kifaa maalum cha mafunzo ya anga kwa wahudumu wa ndege (Full Motion Cabin Crew Mock Up), kununua ndege moja yenye injini mbili ya kufundishia marubani, kujenga kampasi kwa ajili ya kufundisha watalaamu wa bahari na mafuta/gesi katika mkoa wa Lindi na kukamilisha ujenzi wa jengo la maktaba – NIT Mabibo.” amesema Profesa Makame

Katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imeomba kupatiwa zaidi ya shilingi trilioni 3.8 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake mbalimbali.