Profesa Lipumba amtabiria ushindi Rais Samia 2025

0
274

Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba amesema anavutiwa na utendaji kazi wa Rais Samia Suluhu Hassan, hasa kutokana na kuwa msikivu kwa makundi mbalimbali.

Lipumba ameyasema hayo wakati wa mkutano wa hadhara katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa akiwahutubia wakazi wa mkoa huo.

Amesema mikutano aliyoifanya Rais Samia na vyama vya siasa ni kielelezo cha kuonesha demokrasia ya kweli na kuongeza kuwa akiendelea hivyo atajiweka katika nafasi nzuri ya kuchaguliwa kuliongoza tena Taifa mwaka 2025.

“Nakuomba jiwekee lengo la kushinda tuzo ya Mo Ibrahim kwa kuheshimu haki za binadamu na misingi ya demokrasia ya kweli kama unavyofanya sasa, ukiendelea kufanya hivi nina uhakika utarudi tena kuwa Rais wa Tanzania mwaka 2025.” amesisitiza Profesa Lipumba

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan alipolihutubia bunge kwa mara ya kwanza alisema nchi ni ya watu wote na kama kuna mambo ya kuongea yupo tayari kukutana na makundi yote, jambo ambalo amelitekeleza.

Aidha amewashauri viongozi wa mikoa na wilaya nchini kuiga mfano wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuandaa utaratibu wa kukutana na wanasiasa ili kujadili masuala mbalimbali.