Bashungwa amshukuru Rais kwa kuongeza mishahara

0
204

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (TAMISEMI) Innocent Bashungwa amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza kima cha chini cha mishahara ya watumishi wa umma kwa asilimia 23.3.

Akitoa salamu za TAMISEMI kwenye uzinduzi wa barabara Tabora – Koga – Mpanda, Waziri Bashungwa amesema, asilimia 75 ya watumishi wanatoka kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa, hivyo amemuahidi Rais kufanyakazi kwa weledi katika kuwatumikia wananchi.

Waziri Bashungwa pia amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza bajeti ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) katika halmashauri ya wilaya ya Sikonge hadi kufikia asilimia 193 na kubadilisha mandhari ya eneo hilo.

Kwa upande wa ujenzi wa hospitali ya wilaya katika halmashauri ya wilaya ya Sikonge, Waziri Bashungwa amesema serikali ilitoa shilingi bilioni 1.1 na shilingi milioni 180 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi wa afya.