Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeridhia wabunge 19 waliokuwa wanachama wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na baadaye kufukuzwa uanachama
kuendelea na ubunge mpaka maombi yao ya kibali cha kufungua kesi kupinga uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho ulioridhiwa na Baraza Kuu wa kuwafukuza uanachama yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Uamuzi huo umetolewa jioni ya leo na Jaji John Mgeta wa Mahakama Kuu baada ya wabunge hao kuwasilisha
mahakamani hapo shauri la kupinga kufukuzwa uanachama na CHADEMA.
Mapema hii leo, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania DKt.Tulia Ackson aliliambia bunge kuwa kwa sasa hawezi kutamka kuwa viti 19 vya wabunge hao vipo wazi, kwa kuwa suala hilo lipo mahakamani.
Alisema kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki ni mahakama.