Serikali kuwasaidia watoa huduma kwenye sherehe

0
366

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa amesema huu ni wakati wa kuongeza ubunifu katika utendaji kwa tasnia ya utoaji wa huduma kwenye sherehe, ili kutoa ajira na kuongeza kipato cha wanaoshughulika na kazi hizo.

Waziri Mchengerwa ametoa kauli hiyo mkoani Dar es Salaam wakati wa kilele cha maonesho ya tano ya biashara yanayowajumuisha watoa huduma kwenye sherehe.

Watoa huduma hao ni pamoja na washereheshaji, wauzaji wa nguo za harusi, wapishi, wapiga picha, wamiliki wa saluni na watengenezaji keki.

Kuhusu Serikali kutoa mikopo kwa watoa huduma kwenye sherehe, Waziri Mchengerwa amesema tayari Rais Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili yao.

Amewataka kuwasilisha maandiko Serikalini kupitia mashirikisho yao ili waweze kupata mikopo hiyo bila riba yoyote.

Kuhusu kuwa na kumbi kwa ajili ya watoa huduma kwenye sherehe, Waziri huyo wa Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema kuwa, Serikali ina mpango wa kujenga ukumbi wa sanaa na maonesho mkoani Dar es Salaam ambao utakuwa na uwezo wa kuchukua takribani watu elfu ishirini kwa mara moja.