Waliobeba mwili wa Shireen washambuliwa na vikosi vya Israel

0
1377

Wanajeshi na Polisi wa Israel wamepambana na waombolezaji wa Kipalestina ambao walikuwa wamebeba mwili wa mwandishi wa habari wa kituo cha Al Jazeera, Shireen Abu Akleh aliyeuawa kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel huko Jenin katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Mapambano hayo yametokea Mashariki mwa Mji wa Jerusalem, ambako mwili wa mwandishi huyo unazikwa baada ya mamia ya wananchi wa Palestina kuuaga kwa heshima za kitaifa.

Mwandishi huyo wa habari ameuawa akiwa na waandishi wa habari wenzake wakiwa wanapiga picha na kuandika habari ya kile ambacho majeshi ya Israel yalikuwa yamekwenda kufanya kwenye eneo la Jenin, huku wakiwa wamevalia mavazi yanayoonesha kazi yao, ambapo kisheria huwa hawapaswi kushambuliwa.

Huko nchini Uingereza, Wananchi wameandamana nje ya makao makuu ya Shirika la Utangazaji la nchi hiyo BBC jijini London, kupinga mauaji ya mwandishi huyo wa habari wa kituo cha Al Jazeera.

Nao Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kufanyika uchunguzi huru kuhusu mauaji hayo ya Shreen Abu Akleh aliyekuwa na umri wa miaka 51, ambapo tayari Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Uhalifu imepokea kesi kadhaa za mauaji ya waandishi wa habari yaliyofanywa na wanajeshi wa Israel.