Rais wa UAE afariki dunia

0
248

Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Sheikh Khalifa Bin Zayed Al Nahyan, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 73.

Sheikh Khalifa ambaye pia alikuwa mtawala wa Abu Dhabi, amekuwa akionekana mara chache hadharani toka mwaka 2014 alipopata maradhi ya kiharusi.

Kwa mujibu wa katiba ya Umoja wa Falme za Kiarabu, Makamu wa Rais wa UAE Sheikh Mohammed bin Rashid al-Maktoum ambaye ni mtawala wa Dubai atakaimu nafasi ya Urais mpaka hapo Baraza la umoja huo linalojumuisha watawala wa falme saba watakapokutana ndani ya kipindi cha siku 30 kumchagua Rais mpya.

Falme hizo ni Abu Dhabi, Dubai, Sharjah, Ras Al Khaimah, Ajman, Umm Al Quwain na Fujairah.

Sheikh Khalifa aliyezaliwa mwaka 1948, aliingia madarakani mwaka 2004 na kuwa mtawala wa Abu Dhabi na baadaye akawa Rais wa Umoja wa Falme hizo za Kiarabu.

Ndugu wa Sheikh Khalifa Bin Zayed Al Nahyan, Mwana Mfalme Sheikh Mohammed bin Zayed al-Nahyan anatarajiwa kuchukua nafasi ya mtawala wa Abu Dhabi.