Serikali imeahidi kutenga fedha kwa ajili ya kuwapa miradi ya ujenzi makandarasi wazalendo ikiwa ni sehemu ya kuwajengea uwezo kutekeleza miradi mikubwa huku ikiwataka wawe waaminifu.
Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Pof. Makame Mbarawa, wakati akifungua mkutano wa mashauriano kwa makandarasi wa ndani unaoendelea mkoani Dodoma.
“Nitamuomba Rais Samia suluhu Hassan atoe fedha kwa miradi mikubwa itakayotekelezwa lakini mkipewa kazi naomba muwe na bei halisi ambazo hazitatutisha na tunataka kuona thamani ya fedha ili tuone umuhimu wa kuwapa miradi,” alisema
Waziri Mbarawa amesema makandarasi wanawajibu wa kuinua uchumi wa nchi hivyo wanapaswa kutambua jukumu hilo wanapopewa miradi kwani wakichelewesha au kufanya chini ya kiwango wanakwamisha maendeleo ya nchi na kuwakosesha wananchi haki ya kutumia miradi hiyo kwa wakati.
“Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) mmezungumzia Force account sasa nawaagiza tumieni wataalamu wenu kufanya utafiti kama sababu zilizoifanya serikali kutumia utaratibu huo zipo au hazipo, serikali ya awamu ya sita ni sikivu na kama hakuna haja ya kutumia utaratibu huo tutawapa kazi nyingi ila muwe waaminifu,” alisema
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya CRB, Consolata Ngimbwa aliiomba serikali kuachana na utaratibu wa Force Account na kuwapa makandarasi wa ndani kufanya miradi hiyo kwani wengi wao kwa kukosa kazi wako kwenye hali mbaya.
Alisema makandarasi wa fani ya ujenzi waliosajiliwa na bodi wako zaidi ya 4,000 na wamiliki wake wameathirika wao na wategemezi wao kwa kiwango kikubwa kutokana na kukosa kazi kwa muda mrefu na wengine wameshakata tamaa.