Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini Ghana (FDA) imeufunga mgahawa wa Marwako katika mji wa East Legon, kufuatia kuenea kwa taarifa za kuwepo kwa sumu ya chakula kwenye baadhi ya vyakula vinavyouzwa mgahawani hapo.
Taarifa za madai ya kuwepo kwa sumu hiyo ilisambaa kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na hivyo kuzusha hali ya wasiwasi miongoni mwa wateja.
Kufuatia taarifa hiyo, FDA ililazimika kuufunga mgahawa huo ambao ni wa vyakula vya haraka ili kufanya uchunguzi.
“FDA imezingatia malalamiko kutoka kwa umma kuhusu madai ya sumu ya chakula katika tawi la East Legon la mgahawa wa Marwarko na tumefunga mgahawa huo, pamoja na mashirika mengine husika tumeanza uchunguzi,” FDA Imesema katika taarifa yake
Wateja wengi waliopata huduma ya chakula siku za hivi karibuni kwenye mgahawa huo wa Marwako uliopo katika mji wa East Legon, Ghana wamedai kuwa, walianza kuugua mara baada ya kula chakula hicho, hali iliyosababisha baadhi yao kulazwa hospitalini.
Baadhi ya wateja waliodhurika wamesema watafungua kesi mahakamani kufuatia huduma mbovu ya chakula wanayodai kupatiwa mgahawani hapo.