CAG awaponza watumishi MSD

0
205

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amefanya ziara katika Bohari ya Dawa (MSD) na kuagiza watu wote waliohusishwa na tuhuma za ubadhirifu zilizoainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wachukuliwe hatua.
 
Majaliwa amesema hoja zote zilizotolewa katika ripoti ya CAG lazima zifanyiwe kazi na tayari Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeanza kufanyia kazi hoja zote zilizotolewa kuhusu MSD.
 
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa MSD baada ya kutembelea viwanda vinavyotengeneza barakoa na dawa vilivyopo Keko jijini  Dar es salaam.
 
Akizungumzia kuhusu baadhi ya hoja za CAG, Waziri Mkuu amesema MSD ilifanya ununuzi wa vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni tisa (9) bila ya mikataba halali jambo ambalo si sahihi.
 
Pia, Waziri Mkuu amesema taasisi hiyo ilifanya malipo yenye thamani ya shilingi bilioni 3.52 kwa wazabuni sita (6) bila ya kufuata utarabu na wala kuitaarifu bodi ya zabuni ya MSD.
 
Ameongeza kuwa MSD ilifanya zabuni 23 zenye thamani ya shilingi bilioni 8.55 nje ya mfumo wa ununuzi wa TANeps unaosimamiwa na PPRA kinyume na matakwa ya sheria ya ununuzi.
 
“MSD ilifanya malipo ya awali kiasi cha shilingi bilioni 14.89 kwa wazabuni watano (5) bila ya mikataba yoyote au makubaliano mengine ambayo yanabainisha msingi wa malipo ya awali.”
 
Amewataja wazabuni hao kuwa ni Keko Pharmaceutical Industry; Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini; Nakuroi Investment Company Ltd.; Technical Services and General na Wide Spectrum (T) Ltd.
 
Waziri Mkuu amesema taasisi hiyo iliendesha mchakato wa ununuzi na kutoa mkataba wa kusambaza “Liquid Syrup” wenye thamani ya shilingi milioni 898 bila ya kushirikisha Bodi ya Zabuni ya MSD.
 
Amesema taasisi hiyo ilitumia kiasi cha shilingi milioni 215 kwa ajili ya kugharamia posho ya watumishi watatu waliokwenda China kwenye majadiliano ya kuleta mashine za dialysis kwa siku 61.
 
“Watumishi watatu wameenda China kufanya majadiliano kwa nini wasimtumie Balozi wa Tanzania nchini China kufanya shughuli hiyo. Si utaratibu kukaa siku 61 kwa ajili ya majadiliano tena  bila ya kuhusisha menejimenti ya taasisi.”
 
Waziri Mkuu Majaliwa amesema katika taasisi hiyo kuna udhaifu wa usambazaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi licha ya kuwa wamelipwa. “Lazima mjipange vizuri katika utendaji kazi wenu.”
 
Amesema katika idara ya manunuzi kumebainika kuwepo kwa watumishi ambao si wataalamu, hivyo ameagiza wote 16 ambao si wataalamu waondolewe na kuwekwa watumishi wenye taaluma hiyo.