Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema kinachohitajika hivi sasa ni kuhakikisha kunapatikana suluhu ya kudumu katika mataifa mbalimbali yaliokumbwa na migogoro, ili wakimbizi kutoka katika mataifa hayo warudi nyumbani na kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Dkt. Mpango ametoa kauli hiyo Ikulu Chamwino mkoani Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) hapa nchini, Mahoua Parums.
Amesema kwa upande wake Tanzania imekua mstari wa mbele katika kutafuta muafaka wa amani na utulivu katika nchi zinazokumbwa na migogoro mbalimbali ikiwemo vita, lengo likiwa ni kupunguza idadi ya wakimbizi wanaokimbia nchi hizo.
Makamu wa Rais amemkaribisha Mwakilishi huyo mkazi hapa nchini na kumuahidi kwamba Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi.
Wakati wa mazungumzo hayo Mwakilishi huyo Mkazi wa UNHCR nchini amesema Tanzania imeendelea kuwa nchi muhimu zaidi kwa shirika hilo pamoja na wakimbizi kutokana na kuwa nchi iliopokea idadi kubwa ya wakimbizi kwa miongo kadhaa.
Mahoua Parums amemweleza Dkt. Mpango kwamba mchango wa Tanzania katika kupokea na kuhudumia wakimbizi hautasahaulika, ikiwa ni pamoja na ukarimu wanaopata wakimbizi mahali wanapofikia.