Nape ahimiza wanahabari kuikomboa Afrika

0
301

Wanahabari kuwa mhimili wa nne wa dola wametwishwa jukumu la kuhakikisha rasilimali za Afrika zinabadilika kutoka laana na kuwa baraka kwa kuziwezesha nchi za Afrika na watu wake kunufaika.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani jijini Arusha, ambayo kilele chake ni Mei 3 mwaka huu.

Amesema kwa rasilimali zilizopo Afrika, bara hilo halitakiwi kuwa katika hali ya umasikini uliopo sasa, hivyo waandishi wa habari watumie kalamu zao kufichua maovu yanayokwamisha maendeleo ya Afrika na kutoa habari chanya za bara hilo ili kuboresha taswira yake duniani.

Mbali na hilo amesema serikali inaendelea kushirikiana na bunge kubadili sheria zinazokwamisha ustawi wa sekta ya habari.

Aidha, amelishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), kwa jitihada ambazo limekuwa likichukua katika kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari duniani.

Kauli mbiu ya mwaka huu ikijikita katika changamoto za kidijiti, Waziri Nape amewasihi waandishi wa habari kuona fursa zinazotokana na sayansi na teknolojia, pamoja na kuielimisha jamii namna ya kuziendea fursa hizo kama vile fedha za kidijiti.