Maelfu wamuaga Mwai Kibaki

0
195

Viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Philip Mpango wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, leo  wameshiriki kutoa heshima zao za mwisho na kuuaga mwili wa Rais mstaafu wa Taifa hilo Mwai Kibaki aliyefariki dunia wiki iliyopita.
 
Viongozi wengine waliohudhuria shughuli hiyo iliyofanyika katika uwanja wa Nyayo jijini Nairobi ni Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, Rais Sahle Work Zewde wa Ethiopia, Makamu wa Rais wa Zimbabwe Dkt Constantino Chimwenga, Makamu wa Rais wa Uganda Jessica Alupo, Waziri Mkuu wa Rwanda Dkt . Edwardo Ngirente na Rais wa zamani wa Malawi Joyce Banda.
 
Akitoa wasifu wa Rais mstaafu Kibaki ambaye alikuwa msomi na mchumi, Rais Kenyatta amemwelezea Kiongozi huyo kuwa ni mtu aliyejitolea muda wake mwingi kutafuta mafanikio ya wananchi wake huku mtoto wa marehemu Jimmy Kibaki akimwelezea Baba yake kuwa alikuwa kiongozi bora wa familia.
 
Kwa upande wao Rais Sahle Work Zewde wa Ethiopia na Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini wamesema Mwai Kibaki alikuwa kiongozi wa mfano wa kuigwa.
 
Mwili wa kiongozi huyo ambaye anakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika kukuza uchumi wa Kenya pamoja na sekta ya elimu utazikwa kesho Jumamosi huko Osaya katika kaunti ya Nyeri.