Rais Samia arejea na kapu la mafanikio ya Royal Tour

0
285

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametaja mafanikio lukuki yaliyotokana na ziara yake ya wiki mbili nchini Marekani, ambapo kazi kubwa ilikuwa kuzindua filamu ya Tanzania: The Royal Tour.

Akizungumza katika hafla ya mapokezi leo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (KIA), Rais ametaja mafanikio hayo ikiwa ni pamoja na kuvutia uwekezaji wenye thamani ya shilingi trilioni 11.7 ambao unakusudiwa kuzalisha ajira zaidi ya laki 3.

Aidha, amesema Tanzania na Jimbo la Texas, Marekani zilifikia makubaliano na sasa zinaangalia namna ya kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Tanzania hadi Dallas, hatua ambayo amesema itaongeza idadi ya watalii nchini.

Katika sekta ya afya ameeleza mafanikio aliyopata baada ya kutembelea kiwanda cha SC Johnson Family ambacho kimekubali kukarabati na kutoa vifaa kwa vituo vitatu vya kiuchunguzi Tanzania ambavyo ni Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Kituo cha Utafiti wa Afya na Maendeleo Ifakara na Kituo cha Utafiti wa Magonjwa Amani, Tanga.

Pia, kiwanda hicho kimeridhia kujenga vituo vya afya 200 vyenye kila kitu katika mikoa mikoa mitano inayosumbuliwa zaidi na malaria ambayo ni Geita, Katavi, Ruvuma, Kagera na Kigoma.

Kuhusu Royal Tour amesema ameitangaza sana Tanzania kwani kwa nchi moja tu waliyokwenda ameona Tanzania bado haikuwa inafahamika, hivyo jitihada zaidi zinaitajika ili nchi pamoja na vivutio vilivyopo vijulikane duniani.