Rais Samia Suluhu Hassan amesema idadi ya Watalii wanaofika nchini kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii imeongezeka kutoka laki sita na elfu 20 mwaka 2020 hadi kufikia zaidi ya laki tisa mwaka 2021, ikiwa ni ongezeko la asilimia 48.6.
Rais Samia Suluhu Hassan amesema hayo mkoani Kilimanjaro wakati akizungumza na wakazi wa mkoa huo, baada ya kuwasili nchini akitokea Marekani na kuongeza kuwa idadi ya Watalii wanaoingia nchini inatarajiwa kuongezeka maradufu.
Amesema kiwango cha fedha za kigeni kutokana na utalii nchini nacho kimeongezeka kutoka dola milioni 714 za Kimarekani mwaka 2020 na kufikia dola milioni 1, 254 za Kimarekani mwaka 2021.
Akiwa nchini Marekani, Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na mambo mengine alishiriki uzinduzi wa filamu ya Royal Tour ambayo inatangaza vivutio mbalimbali vya utalii pamoja na fursa za uwekezeji zilizopo Tanzania.
Baadaye hii leo Rais Samia Suluhu Hassan atashiriki uzinduzi wa filamu hiyo jijini Arusha, uzinduzi utakaofanyika pia Zanzibar na Dar es Salaam kwa siku tofauti.