Waziri Mkuu akagua ujenzi kijijini Msomera

0
249

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza wizara ya Maliasili na Utalii kuendelea kusimamia kwa ukaribu na kuhakikisha shughuli za ujenzi katika kijiji cha Msomera kilichopo Handeni mkoani Tanga zinakamilika haraka.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo alipokagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika kijiji hicho, ambacho kinandaliwa kwa ajili ya wakazi wa Ngorongoro waliokubali kuhamia hapo ili kupisha shughuli za uhifadhi.

Amesema wizara ya Maliasili na Utalii inapaswa kuhakikisha inaendelea kutoa elimu kwa wakazi wa Ngorongoro waliojiandikisha kuhama kwa hiari, kwani jambo hilo ni muhimu kulifanya.

Kwa upande wa wizara ya Mifugo na Uvuvi, Waziri Mkuu Majaliwa ameitaka kuendelea kuandaa mazingira mazuri ya ufugaji kwa kuhakikisha kunakuwa na miundombinu wezeshi ya wafugaji yakiwemo malambo ya kunyweshea mifugo, majosho na ujenzi wa kliniki ya kutibu magonjwa ya mifugo.

Pia, Waziri Mkuu Majaliw amesema kuwa watumishi wote wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) waliojenga katika hifadhi ya Ngorongoro hawataingia kwenye utaratibu wa kupewa nyumba kwa kuwa walivunja sheria.

“Nataka niwaambie watumishi wa NCAA mliojenga kule, tutaondoa nyumba zenu zote kwa sababu mmevunja sheria, kama unajua umejenga anza kuondoka mwenyewe”. amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula amesema tayari wizara hiyo imepokea shilingi milioni 321 kwa ajili ya kufanya mpango wa matumizi bora ya ardhi katika kijiji cha Msomera na mpaka sasa michoro 11 imekamilika ambapo michoro mitano tayari ina viwanja 14,250 na katika hivyo viwanja 5,250 viko kamili.

“Tunatarajia kijiji hiki kitakuwa cha mfano na hata vijiji vingine vitakuja kujifunza hapa. Tulichokifanya kama wizara ni kuhakikisha mpango wa matumizi bora unakamilika.” amesema Waziri Mabula