Rais Samia Suluhu Hassan ameshuhudia utiaji saini wa mikataba saba kati ya makampuni ya Marekani na Tanzania yenye lengo la kufanya biashara na uwekezaji mkubwa nchini.
Mikataba iliyosainiwa ina thamani ya shilingi trilioni 11.7, na inatarajiwa kutengeneza jumla ya ajira 301,110 kwenye kilimo, utalii, biashara na sekta nyingine za uchumi.
Rais pia ameshuhudia utiaji saini hati za makubaliano (MoU), barua za kuonesha nia (letters of intent) na kuanza kwa mazungumzo ya uwekezaji na biashara kati ya makampuni ya nchi hizo mbili.
Miradi mingine iliyotiwa saini inalenga kuwekeza kwenye mnyororo wa thamani katika kanda ya kaskazini ya sekta ya utalii wa Tanzania, ikiwemo kwenye maeneo ya kutangaza utalii na kuongeza idadi na ubora wa huduma zinazotolewa.
Rais Samia pia ameshuhudia makampuni ya Marekani yakitangaza nia na mipango ya kuongeza mahusiano yao na Tanzania kwenye maeneo ya uwekezaji na biashara. Makampuni hayo ni pamoja na Upepo Energy, Astra Energy, Crane Currency na Parallel Wireless.
Pamoja na mikutano mingine, Rais Samia alihudhuria mkutano kwenye makao makuu ya Chemba ya Biashara ya Marekani (U.S. Chamber of Commerce) uliohudhuriwa na wafanyabiashara na viongozi wa serikali wa nchi zote mbili wakijadiliana namna ya kuongeza uwekezaji na biashara kati ya Tanzania na Marekani.