Waziri Mkuu aipongeza TBC kwa maboresho

0
218

Waziri Mkuu Kasim Majaliwa amesema maboresho yanayoendelea kufanywa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) yameongeza watazamaji na wasikilizaji wa kutokana na kuwashirikisha katika vipindi mbalimbali.

Waziri Mkuu pia ametoa pongezi kwa TBC kwa namna walivyoboresha vipindi vyake na kuongeza usikivu wa redio zake jambo ambalo amelielezea kujisogeza karibu na wananchi.

Akisoma hotuba ya Waziri Mkuu katika hafla ya Uzinduzi wa Jengo la Studio za TBC2 na uzinduzi Rasmi wa Kipindi cha Jambo Tanzania, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema, baada ya kazi nzuri ya kuboresha vipindi vya TBC sasa ni wakati wa kuanzisha Chaneli mahususi ya Michezo.

Aidha ameitaka TBC kuanzisha taarifa ya Habari ya Kiingereza ili kutoa fursa kwa watu wa mataifa mengine kufahamu mambo ambayo Tanzania inayafanya katika kujiletea Maendeleo.

Awali akizungumzia Mradi wa ujenzi wa Jengo la Studio za kisasa la TBC2 na Maboresho yaliyofanyika katika kipindi cha Jambo, Mkurugenzi Mkuu wa TBC Dkt. Ayub Rioba Chacha amesema, lengo la TBC ni kufanya mabadiliko ambayo yatawagusa watu wa rika zote.

Dkt. Rioba ameongeza kuwa, TBC itaendelea kusimamia miradi yake kwa lengo la kuwafikishia wanachi wote taarifa za maendeleo ya nchi yao.