Serikali yatoa Milioni 950 kuboresha huduma za Afya na Elimu Msomera

0
428

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Innocent Bashungwa amesema Serikali imetoa Milioni 500 kuanza ujenzi wa kituo cha afya Msomera katika eneo la mradi wa wakazi wanaotoka katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro na kuhama kwa hiari Wilaya ya Handeni mkoa wa Tanga.

Pia, Serikali imetoa Milioni 400 kuanza ujenzi wa shule mpya za msingi na sekondari na bweni moja katika kata ya Misima katika kiijiji cha Msomera ili wanafunzi wasitembee mwendo mrefu kupata masomo ya elimu ya msingi na sekondari.

Ameyasema hayo leo wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua huduma za msingi za afya, elimu na miundombinu katika eneo la mradi wa wakazi wanaotoka eneo la hifadhi Ngorongoro wanahama kwa hiari katika kijiji cha Msomera wilaya ya Handeni mkoani Tanga.

Bashungwa amesema tayari Serikali imetoa Milioni 50 kwa ajili ya kupanua na kuboresha huduma za afya katika zahanati ya kijiji cha Msomera katika kata ya Misima Wilaya ya Handeni mkoa wa Tanga kinachotoa huduma kwa wananchi wasiopungua 10,000.

Aidha, Bashungwa amesema Serikali itaboresha shule ya Msomera kwa kuongeza vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na kuongeza walimu kutoka na upungufu uliopo kwa sasa katika shule hiyo.