CCM yamuunga mkono Kipanya

0
220

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo ametoa muda wa siku saba kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kufika katika kiwanda cha uzalishaji magari cha Alli Masoud maarufu Masoud Kipanya, kufanya ukaguzi na kutoa vibali vinavyohitajika ili kuruhusu uzalishaji.

Chongolo ametoa muda huo mara baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya kiwanda hicho kilichopo mkoani Dar es Salaam.

“Naiagiza TBS ndani ya siku saba ije hapa ili kukamilisha taratibu za usajili na kukipatia kiwanda hati za ithibati, kwetu hili sio dogo kwa kuwa ilani imeelekeza na kutoa msukumo katika kukuza ubunifu, nikuahidi nitakushika mkono na kufanya harambee na wadau waunge mkono juhudi hizi kwa kukujengea uwezo wa kifedha katika kukiimarisha kiwanda hiki.” amesema Chongolo

Ameahidi ndani ya siku 14 atarejea kiwandani hapo akiwa na taasisi zote zinazohusika na udhibiti wa ubora, lengo likiwa ni kuharakisha mchakato wa kiwanda hicho kuendelea.

Katibu Mkuu huyo wa CCM amesema ilani ya chama hicho imeahidi na imeendelea kuweka msukumo katika ubunifu, hivyo akiwa mtendaji mkuu atahakikisha wanathamini mchango wa wazalishaji wa ndani kikiwemo kiwanda hicho kwa kuwa ni muhimu katika kuongeza ajira kwa Wananchi, kukuza teknolojia na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni.

Amemtaka Masoud kuendeleza ubunifu huo na asivunjike moyo, kwani CCM pamoja na Serikali vipo pamoja naye wakati wote.

Kwa upande wake Kipanya amesema, wazo la uzalishaji wa kiwanda hicho ni mchakato ulioanza mwaka 2013 ambapo alifanya usajili na kuanza uzalishaji wa kwanza mwaka 2020.