Treni kutumia saa 6 kutoka Dar – Tabora

0
284

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha Makutupora -Tabora utagharimu shilingi trilioni 4.606.

Akizungumza mkoani Tabora wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa reli hiyo, Kadogosa amesema ujenzi huo unatarajiwa kutumia muda wa miezi 42 inayojumuisha miezi minne ya majaribio.

Amesema matarajio ni kwamba ujenzi wa reli hiyo ya kisasa kipande cha Makutupora -Tabora utakamilika mwezi oktoba mwaka 2025.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu huyo wa Shirika la Reli Tanzania, treni zitakazotumia reli hiyo ya kisasa zitakuwa zikisafiri kwa umbali wa kilomita 160 kwa saa kwa treni ya abiria na za mizigo zitasafiri umbali wa kilomita 120 kwa saa.

Kwa upande wa treni ya abiria, itatumia muda wa saa sita kutoka Dar es Salaam hadi kufika Tabora badala ya saa 20 mpaka 36 zinazotumiwa na treni za kawaida hivi sasa.

Jiwe la msingi la ujenzi wa reli hiyo ya kisasa kipande cha Makutupora -Tabora limewekewa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa.