Handeni kuwa ya mfano ufugaji wa kisasa

0
237

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amesema kuwa Serikali imeweka mipango mizuri ya kuhakikisha kijiji cha Msomera kilichopo wilayani Handeni mkoani Tanga kinakuwa na miundombinu ya kisasa ya kuhudumia mifugo ikiwemo majosho, malambo na nyanda za malisho. ili wafugaji kutoka hifadhi ya Ngorongoro watakaohamia katika eneo hilo waweze kufuga kisasa.

Naibu Waziri Ulega ametoa kauli hiyo alipofanya ziara katika kijiji hicho ambapo kuna eneo lililotengwa maalum kwa ajili ya Wafugaji kutoka hifadhi ya Ngorongoro kuhamia hapo kwa hiari ili kuendeleza shughuli zao za ufugaji.

Baada ya kukagua maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho, majosho na malambo, Naibu Waziri Ulega amewaelekeza wataalam wanaosimamia uendelezaji wa maeneo hayo kuweka mikakati mizuri ya kukamilisha ujenzi wa miundombinu hiyo, ili wafugaji hao kutoka Ngorongoro watakapohamia eneo hilo wakute miundombinu ipo tayari na waweze kuendelea na shughuli zao.

“Tunataka wafugaji watakaokuja kufanya shughuli zao katika kijiji hiki cha Msomera wafanye shughuli zao za ufugaji kisasa, wafanye ufugaji wa kibiashara na tunataka hapa pawe ni shamba darasa ili hata mtu akitaka kujifunza ufugaji wa kisasa aletwe hapa.”amesema Naibu Waziri Ulega