Serikali imeahidi kupunguza viwango vya kodi kwa baadhi ya bidhaa muhimu zinazoingia nchini ikiwa ni pamoja na bidhaa za sukari, mafuta ya kula na petroli, lengo likiwa ni kudhibiti kuendelea kupanda kwa bei za bidhaa.
Ahadi hiyo ya Serikali imetolewa mkoani Dar es Salaam na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba wakati wa mkutano na waandishi wa habari, mkutano uliolenga kuangazia mwenendo wa uchumi na mfumuko wa bei za bidhaa uliosababishwa na UVIKO – 19 pamoja na vita baina ya Russia na Ukraine.
Akitoa ahadi hiyo Dkt. Nchemba amesema, miongoni mwa hatua za haraka ambazo zitachukuliwa na Serikali ni kupunguza viwango vya kodi kwa asilimia isiyozidi kumi kwa waagizaji wa sukari na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA kuweka viwango vipya vya kodi kwenye mafuta ili kutoa ahueni kwa Watanzania.
Waziri huyo wa Fedha na Mipango amewasihi Watanzania kuendelea kuunga mkono dira ya Serikali, kwa kuendelea kufanya kazi Ili kusaidia nchi kuwa na uchumi endelevu kwa kuongeza uwekezaji kwenye sekta za kilimo, Uvuvi na Ufugaji.