Rais Samia: Tunaimarisha chama

0
201

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Samia Suluhu Hassan amewaambia wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho kuwa, lengo la mkutano huo ni kuimarisha utendaji wa CCM.

Akifungua mkutano huo katika ukumbi Jakaya Kikwete mkoani Dodoma Rais Samia Suluhu Hassan amesema, wameitisha mkutano huo ili kuifanyia marekebisho Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2020 ili iendane na mahitaji ya chama hicho kwa wakati huu.

Mkutano huo pamoja na mambo mengine utapitisha marekebisho ambayo yataruhusu Makatibu wa mikoa wa chama hicho kuwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) na marekebisho mengine.

Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM pia watapiga kura na kupitisha jina la mgombea nafasi ya Makamu mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, ambapo aliyependekezwa ni aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho Abdulrahman Kinana.