Dkt. Mpango: Maendeleo ya pamoja yapo kwenye kushirikiana

0
228

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango amesema bara la Afrika linapaswa kuwa na ushirikiano mkubwa kupitia mkataba wa eneo huru la kibiashara la Afrika ili kufikia maendeleo ya pamoja na haraka wakati huu wa ufufuaji uchumi baada ya madhara ya UVIKO19.

Makamu Rais amesema hayo leo Machi 30, 2022 wakati wa majadiliano katika Jukwaa la 8 la Wakuu wa Nchi na Serikali Duniani linalofanyika Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu.

Amesema kutoka na Afrika kujaaliwa rasilimali nyingi, nchi za Afrika zinapaswa kushirikiana katika miradi itakayoinua uchumi wa bara hilo ikiwemo miradi ya nishati na miundombinu. Aidha ameongeza kwamba bara la Afrika kabla ya UVIKO19 uchumi wake ulikua ukipanda kwa asilimia 3.3 hadi 3.5 pamoja na kupungua kwa kiwango cha umasikini.

Akizungumzia nchi ya Tanzania, amesema serikali inaendelea na jitihada za kuimarisha uchumi ikiwemo kuchukua hatua za kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi kwa manufaa ya pande zote mbili.

Halikadhalika Makamu wa Rais amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abudhabi, Mohamed Seif Al Suwaidi ambapo wamezungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano katika miradi inayotekelezwa na mfuko huo nchini Tanzania.