Dkt. Mpango asisitiza ulinzi chanzo cha maji Mzakwe

0
364

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amelitaka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kikosi namba 834 Makutupora kilichopo mkoani Dodoma, kupanda miti pembezoni mwa barabara ya kuingia jiji la Dodoma ili kuhifadhi mazingira pamoja na kupendezesha eneo hilo.

Makamu wa Rais amesema hayo alipotembelea eneo hilo la JKT Makutupora, ambapo amesisitiza uwepo wa kambi hiyo ya jeshi katika eneo hilo ni kwa sababu ya ulinzi wa chanzo cha maji katika bonde la Mzakwe hivyo wanapaswa kufanya uhifadhi huo kikamilifu.

Aidha, amekiagjza kikosi cha JKT Makutupora kuhakikisha kinadhibiti waharibifu wa mazingira na waoingiza mifugo na kuchoma mkaa jirani na chanzo hicho cha maji cha Mzakwe.

Amesema Serikali imeweka mkazo katika uhifadhi wa mazingira, na tayari imeleekeza upandaji miti katika ngazi za kaya ambapo kila kaya inapaswa kupanda miti mitatu hadi mitano kulingana na maeneo husika.

Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Brigedia Jenerali Rajabu Mabele amesema jeshi hilo litatekeleza kikamilifu maagizo hayo na kuweka mkazo katika uhifadhi wa eneo hilo na sehemu zingine zinazohusika na JKT.